NEW ALERT

recent
MAHABA

MWANAMKE WA KIISLAMU YAFANYE HAYA






1. MWANAMKE WA KIISLAMU ni mwenye kuamini Allah mtukufu kuwa ndie Mola wake wa haki, na kuwa Muhammad (s.a.w) ni Mtume wake, na kuwa Uislamu ndio Dini yake, basi anakuwa ni mwenye kutokeza kwake athari za Imani yake kwa Maneno, Matendo na Itikadi, anakuwa ni mwenye hadhari kubwa yasije yakamchukuwa Makasiriko ya Allah mtukufu, ni mwenye kuogopa Maumivu ya Adhabu yake na Ubaya wa kwenda kinyume na Amri zake, amesema Mtume Muhammad (s.a.w): ((Sio Imani kwa kutamani, lakini Imani ni ile aliyotulizana katika Moyo na ikasadikishwa na Matendo)).


2. MWANAMKE WA KIISLAMU anahifadhi Sala tano kwa Udhu wake katika wakati wake, wala hashughulishwi na chochote akawacha Sala, wala hababaishwi na Mila yoyote akawacha Ibada, basi idhihirike kwake athari ya Sala, kwani hakika ya Sala ni yenye kukataza machafu na maovu, basi hii ndio hifadhi kubwa ya kumlinda na Maasi, amesema Mtume Muhammad (s.a.w): ((Munaona vipi,, ikiwa mbele ya mlango wa mmoja wenu pana mto wa maji, na akawa anakoga ndani yake kila siku mara tano hivi kitabakia kitu katika uchafu wake?)) Wakasema: Hakibakii kitu katika Uchafu wake. Akasema (s.a.w): ((Basi huo ndio Mfano wa hizi Sala tano)).


3. MWANAMKE WA KIISLAMU anahifadhi Hijabu yake na anajitukuza kwa kujishika nayo vizuri, basi yeye hatoki nje isipokuwa amejihifadhi kwa heshima za Dini yake, akitaka hifadhi ya Mola wake kwa kumkirimu na kumlinda yeye kwa pambo la Hijabu, na akataka kumtakasa kwa tabia bora, amesema Allah mtukufu ((Ewe Nabii,, Waambie Wake zako na Watoto wako wa kike, na Wanawake wa Waumini, wajishike vizuri kwa kujilazimisha juu yao Majil-babu (Nguo mzito zinazoficha mapambo yote ya maumbile ya mwanamke) hilo ndio ukaribu zaidi wa kujulikana wasije wakafanyiwa maudhi na amekuwa Allah ni mwingi wa kusamehe mwingi wa kurehemu)) [Ah-zaab 59]


4. MWANAMKE WA KIISLAMU anajitahidi katika kumtii Mume wake, basi anakuwa ni mwepesi katika kutimiza haki zake, anamrehemu na kumuita kunako mambo ya kheri na anamnasihi na kutaka nasaha kwake, anafanya kwa Mume wake yale yanampendezesha, na wala hanyanyui sauti yake juu ya Mume wake na hazungumzi na yeye kwa ukali, amesema Mtume Muhammad (s.a.w): ((Atakaposali Mwanamke Sala zake tano, na akafunga mwezi wake, na akamtii Mume wake ataingia katiia Pepo ya Mola wake kwa mlango atakaotaka)).


5. MWANAMKE WA KIISLAMU anawalea Watoto wake malezi mema ya kumtii Allah mtukufu na Mtume wake Muhammad (s.a.w), anawanyonyesha Itikadi sahihi ya Uislamu, anaotesha katika mioyo yao Mapenzi ya Allah mtukufu na Mtume wake Mkarimu Muhammad (s.a.w), na anafanya kila juhudi ya kuwaepusha na kuwahadharisha kunako Maasi na Tabia mbaya, amesema Allah mtukufu: ((Enyi ambao mumeamini,, Okoweni Nafsi zenu na watu wenu kunako Moto, kuni zake ni watu na mawe, uwewekewa Malaika wasio kuwa na huruma walio wakali hawamuasi Allah kwa aliyowaamrisha na wanafanya yote waliyoamrishwa)) [Tahriim 6].


6. MWANAMKE WA KIISLAMU hakubali kuwa pamoja na Mwanamme wa kando([1]) peke yao, amesema Mtume Muhammad (s.a.w): ((Hawatokaa Mwanamme na Mwanamke peke yao isipokuwa Shetani atakuwa ni wa tatu wao)). Basi yeye hatosafiri isipokuwa na Maharimu wake au Mume wake na wala havamii masoko na sehemu za makusanyiko ya watu isipokuwa kwa dharura inayokubalika kisheria, tena akiwa ni mwenye Hijabu yake na heshima zake amejisitiri kwa pambo la Uchamungu.


7. MWANAMKE WA KIISLAMU hajifananizi na Wanaume katika yanayowahusu, wala haunganisi nywele zake, wala hanyowi wala kupara nyusi zake, wala hachongi meno yake, wala haweki chapa katika mwili wake, wala hajifananishi na Wanawake Makafiri katika yanayowahusu kwa nguo zao na sehemu zao na namna zao, amesema Mtume Muhammad (s.a.w): ((Amelaaniwa na Allah mwenye kuchonga nyusi zake na mwenye kuifanya kazi hiyo, na mwenye kuunganisha nywele zake na mwenye kifanya kazi hiyo, na mwenye kujipiga chapa katika mwili wake na mwenye kuifanya kazi hiyo, mwenye kuchonga meno kwa kutaka uzuri wa mwanya , kama alivyowalaani wanawake wenye kujifananisha na Wanaume, na wanaume wenye kujifananisha na Wanawake)), na amesema: ((Mwenye kujifananisha na watu fulani basi huyo atafufuliwa pamoja na wao)).


8. MWANAMKE WA KIISLAMU ni mwenye kuita Wanawake wenzake katika Kumtii Allah mtukufu na Mtume wake Muhammad (s.a.w) kwa maneno mazuri na vitendo vyema, na kwa kuwatembelea majirani zake, jamaa zake, ndugu zake na kuwazawadia zawadi za kuwaongoza katika njia anayoiridhia Allah mtukufu. Na hali yeye mwenywewe ni mwenye kufanya kwa yale anayoyasema na kuyahimiza ili kuiokowa nafsi yake na wenzake kunako Laana na Makasiriko na Adhabu ya Allah mtukufu. Amesema Mtume wa Allah (s.a.w): ((Kwa hakika kumuongoa Allah mja yoyote kwa sababu yako ni bora kwako kuliko ngamia wekundu)).

9. MWANAMKE WA KIISLAMU anahifadhi Moyo wake kunako yenye kubabaisha na yenye matamanio, pia anahifadhi jicho lake kuona mambo ya haramu, na sikio lake kusikiliza ya haramu kama muziki, upuuzi, na machafu ya kuteta na fitina na matusi…. Na anahifadhi viungo vyake vyote kunako kufanya maasi na huku anajuwa kuwa huo ndio Uchamungu, amesema Mtume Muhammad (s.a.w): ((Oneni haya kwa Allah mtukufu, na mwenye kumuonea haya Allah mtukufu haki ya kumuonea haya hakika atahifadhi kichwa chake na yanayokifika, na atahifadhi tumbo lake na yanayoingia, na atakayekumbuka mifupa ya kaburini hatodanganywa na mapambo ya Duniani)).


10. MWANAMKE WA KIISLAMU anahifadhi wakati wake usipotee bure, na mchana wake na usiku wake usije ukachanika ovyo, basi yeye ni mwenye kujitenga na kusengenya (kuteta), Ulimi mrefu, sauti refu, matusi, dharau, kujisahau ovyo, kupumbazika na mavutio ya kinafsi, amesema Allah mtukufu: ((Na waache wale ambao wamefanya Dini yao kuwa ni Michezo na Mapumbazo ya kinafsi, na yakawadanganya maisha ya kidunia, na wewe kumbusha kwa hilo, isije ikaangamizwa nafsi kwa yale iliyochuma, nayo haina asiyekuwa Allah kipenzi wala muombezi, na hata ikitolewa kila fidia haitokubaliwa kwake, hao ndio walioangamizwa kwa sababu ya yale waliyochuma, watapata wao kinywaji cha maji yenye kuchemka mno na adhabu yenye kuumiza kwa walivyokuwa wakikifuru)) [An-aam 70] na amesema Allah mtukufu kwa kuwazungumzia wale waliopoteza Maisha yao ya kuwa watajuta huku wakisema ((Ee,, OLE wetu kwa tulivyopuuza! Na wao watabeba mizigo yao juu ya migongo yao, Ee,, ifahamike kuwa ni maovu mno hayo wanayoyabeba)) [An-aam 31].


NDUGU YANGU WA KIKE HEBU KUWA NGUVU YA HAKI KATIKA JAMII KWA YALE ANAYOIRIDHIA ALLAH MTUKUFU AMBAYE AMEKUUMBA WEWE NA KILA KITU, NA USIWE NGUVU YA BATILI YA NAFSI NA SHETANI WA KIJINI NA WATU UTAANGAMIA NA KUANGAMIZA JAMII YAKO.

EWE MOLA MUONGOZE MWAMKE WA KIISLAMU KWA YALE UNAYOYAPENDA NA UKAYARIDHIA NA UUPE MOYO WAKE NURU YA IMANI YA KWELI (AMIN).

Alisema Mtume wa Allah (s.a.w): ((Makundi mawili ya walio wa motoni sijayaona bado, wanaume katika mikono yao kuna bakora kama mikia ya n`gombe wanapiga watu ovyo, na wanawake wamevaa lakini wako uchi wanatembea kimaringo vichwa vyao kama nundu za ngamia ziliyoinama, hawatoingia peponi wanawake hao, wala hawatapata hata harufu yake, na hakika harufu yake inapatikana masafa kadha wa kadha)).

MWANAMKE WA KIISLAMU YAFANYE HAYA Reviewed by Admin on 2:30 PM Rating: 5

No comments:

All Rights Reserved by . © 2020
credit JOJOThemes

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.